Header Ads

MSONGAMANO WAWAGONJWA KILIO CHA WAUGUZI RUFAA MBEYA



Mbeya.Wauguzi wa  Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya  wamelalamikia  uwepo wa msongamano wa wagonjwa wodini na kwamba unasababisha utoaji wa huduma kuwa mgumu hususani kwa wagonjwa wanolala chini.

Walitoa malalamiko hayo, jana katika risala yao  ya kuadhimisha   siku ya wauguzi duniani ambapo siku hiyo waliitumia kuchangia mifuko 257 ya saruji  yenye thamani Sh3.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la watoto  na fedha tasilimu Sh800,000 kwa ajili ya mahitaji ya chakula kwa wazee.


Akisoma risala hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntinika, kwa niaba ya wauguzi wenzie,Ofisa Muuguzi Msaidizi Joyce Komba alisema msongamano huo ni hatari kwa wagonjwa na wauguzi na kwamba huweza kumpelekea mgonjwa kuambikizwa magonjwa.

"Hali hii ya msongamano tuanaomba serikali ilifanyie kazi kwa ukaribu kwani humsababishia mgonjwa kupata magonjwa mbali mbali ambayo humfanya akae kwa muda mrefu hospitalini na pia anakosa haki yake ya usiri"alisema
 
Alisema pamoja na changamoto hiyo lakini pia wauguzi hao wanakabiliwa na tatizo la  kutopandishwa  vyeo kwa wakati ,ukosefu wa baadhi ya vifaa tiba,ukosefu wa nyumba za kuishi  na  fedha zinatolewa kwa ajili ya sare za kazi ni ndogo kulingana na gharama za maisha.

"Wauguzi tumekuwa  na tatizo kubwa la ukosefu wa nyumba karibu na mahala pa kazi,hali hii imetupa wauguzi wakati mgumu  katika utekelezaji wa majukumu yetu"alisema 

Aidha  alisema wanaiomba serikali kuwapatia stahiki zao ikiwepo kupandishwa vyeo kwa wakati ili kuleta motisha na morali wa kufanya kazi ikiwa ni pamoja na  serikali kuajiri wauguzi wa kutosha  ili kuongeza ufanisi wa kazi na uwiano wa wauguzi na wagonjwa tunaowahudumia.

Alisema kuwa serikali iongeze fedha za sare za kazi kutoka Sh 120,000 hadi 300,000 na kwamba iwafikirie kuwagawiwa viwanja kwa bei nafuu ili waweze kujenga nyumba zao wenyewe na kupunguza adha ya ukosefu wa nyumba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa hospitali ya kanda ya Mbeya Dk Godlove Mbwanji alisema  wauiguzi wanachangamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi  nyingi na zaidi ya muda unaotakiwa hivyo  jamii inatakiwa kutambua umuhimu wa kazi wanayoifanya.

Kuhusu ujenzi wa jengo hilo la watoto alisema kuwa umegharimu kiasi cha Sh 370milioni kwa kuwatumia mafunzi wa kawaida na kwamba endapo wangetumia kampuni ya ukandarasi  gharama yake ingekuwa Sh650 milioni.

Akizungumza mara baada ya kupokea mifuko hiyo Saruji Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntinika amewataka wauguzi hao kufanya kazi kwa kufuata  maadili ikiwa ni pamoja na kutoa huduma nzuri kwa wateja wao ambao ni wagonjwa.

"Tunatambua umuhimu wa kazi yenu ni ngumu sana hivyo  inahitaji  kupewa moyo  kwani  mmekuwa mkihangaika na wagonjwa usiku na mchana katika hilo serikali inawapongeza ,na kwa hatua hii ya kujitoa kuchangia saruji kwa ajili ya jengo la watoto tunawapongeza muendelee na moyo huo huo wa kujitolea hata wakati wa kutoa huduma "alisema 

Mwisho


No comments