MBEYA CITY YATANGAZA VITA KWA YANGA
Mbeya. Klabu ya Mbeya City imesema haitaki kuwa ngazi ya ubingwa kwa Yanga na imeapa kwamba mechi yao itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa lazima Yanga akubali kukaa hata kama atakuwa katika uwanja wake wa nyumbani.
Akizungumza na gazeti hili , Meneja wa City, Geodfrey Katepa alisema kwamba wamekuwa katika maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Katepa alisema kikosi cha City tangu kikosi hicho kirejee kutoka Sumbawanga, ambako kilikuwa kimeweka kambi ya siku tano iliyohusisha pia michezo minne ya kirafiki, ambapo walishinda yote .
“Tumefanya mazoezi ya hapa na pale ili kuona wachezaji wengi wanakuwa fiti kabla ya kwenda Dar es Salaam kuvaana na mabingwa hao watetezi ,”alisema Kiungo huyo wa zamani wa Yanga.
Alisema kwamba wanajiandaa vizuri ili wakaifunge Yanga mjini Dar es Salaam na kujenga heshima dhidi ya mabingwa hao watetezi ambao wanaonekana kuwa mlima kwa timu pinzani pindi zinapocheza uwanja wa Taifa.
“Sisi tunachotaka ni kuwafunga tu, haijalishi kama hatuwi mabigwa au hatushuki. Tunataka heshima ya kuwanyoosha , na tukiwafunga Yanga tutajijengea heshima ya kukwamisha ubingwa wao huo wanaoutaka kwa mwaka huu tena ,hatutaki kuwa ngazi ya ubingwa ya Yanga kila msimu tukicheza nao mechi hizi za lala salama,”alisema.
Kikosi cha wachezaji wa Mbeya City kinatarajia kuondoka jijini hapa muda wowote kwa ajili ya kwenda jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuvaana na Yanga Mei 14 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa.

Post a Comment