Header Ads

NJOMBE MJI KUFANYA KUFURU LA USAJILI MSIMU HUU



Mbeya. Klabu ya Njombe Mji itakayoshiriki ligi Kuu Bara  msimu ujao kwa mara ya kwanza  imesema itafanya usajili wa aina yake kwa kufanya usaili wa wachezaji wanaojiona wana sifa na wako fiti kuitumikia timu hiyo kwenda  mkoani hapo Mei 15 mwaka huu kwa ajili ya zoezi hilo litakalochukua siku tano.

Mwenyekiti wa Klabu hiyo ,Erasto Mpete alisema wanafanya usajili wa aina hiyo ili kuwa na kikosi cha wachezaji wenye uwezo na siyo majina makubwa kwani wamejifunza kwa Klabu kubwa zinazosajili jina na siyo viwango na matokeo ya wachezaji hao wanaboronga uwanjani.


 ''Sifa yake awe anacheza ligi kuu,daraja la kwanza na hata ligi daraja la pili kwani tunataka kuandaa kikosi imara kitakacholeta tija na heshima kwa mkoa wetu na ukizingatia ni mara ya kwanza kwetu kushiriki michuano hii na tunataka tuonyeshe kuwa hatukubahatisha kupanda ligi,''alisema Mpete.

Alisema ''Kuna wachezaji zaidi ya 45 ambao wamechaguliwa na uongozi wa timu  ambao wataungana na wale watakaojitokeza kwa ajili ya usaili kwa kupata kikosi cha wachezaji 25 tu watakaoingia kambini Mei 21 mwaka huu ,''alisema

Alisema hadi sasa kuna idadi ya wachezaji wachache walioingia nao mkataba ingawa hakuwa tayari kutaja idadi na majina yao na kwamba mambo yote yakiwa sawa ndipo watawaweka wazi wachezaji hao.

''Wapo wa kutoka Nigeria,Malawi na Zambia ambao tutakuwa nao kwenye zoezi zima la usaili ili kuona vipaji vyao na katika hili la usajili hatuna undugu wala upendeleo ,tumejipanga kupata kikosi cha uhalali na sisi tunasema 'Njombe Mji ni viwango tu',alisema 

Kuhusu Benchi la ufundi, Mpete alisema  kuwa litaundwa na meneja Damian Mkuye huku kocha mkuu akiwa Hassan  Banyai aliyeipandisha timu hiyo  pamoja na kocha wake msaidizi  Mlage Kabange aliyewahi kuzifundisha timu za  Nazareth (Njombe)na Mbeya Warrios ya jijini hapa.

''Kocha wa magolikipa bado hajapatikana hadi sasa lakini tupo kwenye mazungumzo na watu wawili huku mmoja wa kocha hao akitokea nchini Uganda na endapo tutafikia muafaka na mmoja kati yao basi kila kitu kitawekwa wazi,alisema

Katika hatua nyingine, Mpete alisema  Uwanja watakaoutumia katika michunao hiyo ya ligi kuu ni Sabasaba kutokana na kazi nzuri ya ukarabati inayoendelea kwa sasa  na kamati ya matengenezo ya uwanja huo chini ya Meneja  Filoteus Mligo .

No comments