Mbeya City kutembeza bakuli ni aibu
Mbeya. Mbeya City ni miongoni
mwa klabu zinazozungukwa na neema ya kuwa na udhamini mnono hata kuzipiku timu
Kongwe za Simba na Yanga lakini cha kushangaza timu hiyo kwa sasa choka mbaya.
Achana na udhamini wa Vodacom na
Azam zilizonazo timu zote 16 zilizoshiriki ligi kuu kwa msimu huu lakini wao
(Mbeya City) wana dhaminiwa na Binslum, Sports Master, Cocacola pamoja na
Bhojan Chemistry anayetoa dawa kwa wachezaji pindi wanapoumia.
Lakini cha kushangaza kwa msimu huu
timu hiyo imefikia hatua mbaya kiuchumi,hali iliyowafanya madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambao ndiyo
wamiliki wa timu hiyo kuingilia kati ili kunusuru hali hiyo.
Hali ya ukata kwa siku za hivi karibuni imesababisha kwa
baadhi ya wachezaji kutolipwa mishahara yao ya miezi miwili hadi mitatu na hii
inawezekana ndiyo chanzo haswa cha timu kuvurunda msimu huu.
Kutokana na hilo madiwani waliamua
kuweka mambo wazi kuhusu timu kukabiliwa na ukata na kutakiwa kuichangia klabu
yao kwani bila mabosi hao mambo hayawezi kwenda sawa.
Katika kikao cha Baraza la
madiwani wa halmashauri ya jiji kilichofanyika hivi karibuni ,
Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii wa Mbeya City,Fanuel Kianula
alitangaza mbele ya baraza hilo kuwa kila diwani anatakiwa
kuichangia Klabu kiasi cha Sh20,000 .
Lengo kubwa la madiwani hao
kutakiwa kuchanga fedha ni kwa ajili ya kuisaidia klabu kumaliza msimu vizuri
na kumalizana na wachezaji wao.
Hali ya ukata ilianza kwa mabingwa
watetezi wa ligi hiyo (Yanga) huku jinamizi hilo likihamia kwa Mbeya City
ambayo katika akili za wadau na wapenzi wa soka haiwezi kupenya kwamba klabu
hiyo inatembeza bakuli.
Na hii inaniaminisha kuwa kipindi cha
duru la pili la msimu huu timu
inapovurunda na kupata sare zaidi ya nne mfululizo kuna baadhi ya wachezaji
walidokeza kuwa wanadai mishahara yao lakini pia posho zenyewe ilikuwa shida
kuzipata kumbe ukata ulikuwepo ila viongozi wake walivunga tu kuweka mambo wazi.
Kwa mujibu wa Katibu wa klabu hiyo
Emmanuel Kimbe, inadaiwa kuwa bajeti ya kuendesha timu inagharimu Sh1.2 bilioni
kwa msimu mmoja ,hii ikiwa ni mishahara,posho pamoja na chakula kwa
wachezaji wakiwa kambini.
Najiuliza Mbeya City hii hii
yenye wadhamini hata kuzipiku klabu kongwe hapa nchini za Simba na Yanga
imekuwaje leo hii itembeze bakuli kwa watendaji wake wa halmashuri hata kama
ndiyo wamiliki?
Mapema Aprili mwaka huu imeongeza
mdhamini wanne ambaye ni Sports Master atakayetengeneza na kuuza jezi zao kwa
misimu miwili yaani kuanzia msimu ujao wa ligi .
Mamilioni yanayotolewa na wadhamini
hao yanafanya kazi gani hadi madiwani wake waanze kuichangia timu hiyo
inayotamaniwa na vilabu vingi vinavyopiga miayo ya njaa hapa nchini.
Kwa fikra zangu nilijua huu ni wakati
wa klabu hiyo kupumua kuhusu mambo ya kifedha na sasa ielekeze nguvu na akili
jinsi ya kumaliza mechi hizo mbili zilizoshika majibu ya wao kusalia ama kwenda
na maji.
Lakini tunapata taarifa ya kwamba
ukata uliopo ni balaa labda Mungu tu asimame ili wachezaji wamalize msimu
huu vyema na kila mmoja aondoke akiwa hana dukuduku na mtu .
Haiwezekani kwa timu pendwa kama
Mbeya City kutudanganya leo hii kwamba haina fedha wakati misimu yote mitatu
tangu ianze kushiriki ligi imeendeshwa vizuri kwa nini msimu huu ilie
njaa na huku imeongeza mdhamini mapema.
Na ndiyo maana matokeo ya klabu hiyo
kwa misimu miwili mfululizo siyo ya kuridhisha kwani imekuwa ikipita kwenye
tundu la sindano wakati kwa msimu wake wa kwanza ilizichchafya Simba , na
Yanga kupata matokeo zilipokuna nayo.
Ni wakati wa benchi zima la ufundi
wa klabu hiyo kukaa chini na kujitafakari mara mbili mbili kwamba ukata huo
unatokana na nini?,
Yawezekana kuna wajanja wachache
wanaotumia mwanya huo kujinufaisha wao na kusahau maslahi ya klabu inayouletea
mkoa wa Mbeya heshima ya kipekee pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana.
Ni wakati wa kuamka na kufuta makosa
yote yaliyojitokeza kwa msimu huu ili yasijirudie msimu ujao kwani kulewa sifa
kutatugeuzia kibao na kuwa kama timu ile iliyopanda kwa mbwembwe na kushuka kwa
mbwembwe hadi leo iko wapi ?
Viongozi pamoja na benchi la ufundi
hapo kuna kitu cha kujifunza na kuchukua hatua ikiwemo hii ya kutorudia makopsa
yaliyompata jirani yako Tukuyu Stars amabye hadi sasa amepotea kwenye ramani ya
soka.
Siku zote kuna usemi usema ‘chuki na
ubinafsi ni adui wa maendeleo ’ hivyo vyombo vya dola vinatakiwa viingilie kati
kufanya uchunguzi juu ya suala hili
Post a Comment