UCHAGUZI KENYA WAPINZANI KUMTAJA MGOMBEA
Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya unatarajiwa kumtaja atakayewania urais dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.
Tangazo hilo litafanyika huku nchi hiyo ikimaliza shughuli kura za mchujo za vyama, ambazo zimekumbwa na vurugu na madai ya kuiba kura.
Huku zikiwa zimesalia siku 102 tu kabla ya uchaguzi, muungano mkuu wa upinzani Kenya ulikuwa na muda mdogo kumtaja kiongozi wao. Muungano huo wa National Super Alliance, yaani NASA, una wanaume watano wote wanaotaka kuongoza, lakini inatarajiwa kuwa jopo litamchagua Raila Odinga.
Vigogo wengine kwenye muungano huo ni makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka, makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi, waziri wa zamani wa mambo ya nje Moses Wetangula na mwenyekiti wa zamani wa baraza la magavana Isaac Ruto.
Bw Ruto, anayeongoza chama cha Chama cha Mashinani (CCM) alikuwa kwenye muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Bw Kenyatta kabla ya kuhama na kuunda chama chake.
Bw Odinga ndiye kiongozi wa chama cha ODM, ambacho kina wabunge wengi zaidi katika Bunge la sasa.

Post a Comment